1 Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
2 Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.
3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu.
4 Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.