11 Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia.
12 Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu.
13 Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniondokee na kunivizia kama hivi leo?
14 Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako?
15 Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi.
16 Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako.
17 Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa BWANA, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa BWANA.