5 Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli.
6 Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.
7 Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake.
8 Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi, akamsujudia.
9 Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru?
10 Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi BWANA alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA.
11 Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.