3 Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali.
4 Naye Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia mpaka Gathi; wala hakumtafuta tena.
5 Daudi akamwambia Akishi, Sasa kama nimeona kibali machoni pako na nipewe mahali katika miji hii mmojawapo mashambani, nipate kukaa huko; mbona mtumwa wako akae katika mji wa kifalme pamoja na wewe?
6 Ndipo Akishi akampa Siklagi siku ile; kwa sababu hiyo huo mji wa Siklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hata hivi leo.
7 Na hesabu ya siku alizokaa Daudi katika nchi ya Wafilisti ilikuwa mwaka mzima na miezi minne.
8 Naye Daudi na watu wake walikuwa wakikwea na kuwashambulia Wageshuri, na Wagirizi, na Waamaleki waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo, tangu Telemu, hapo uendapo Shuri, hata mpaka nchi ya Misri.
9 Tena Daudi akaipiga nchi hiyo, asimhifadhi hai mume wala mke, akateka nyara kondoo, na ng’ombe, na punda, na ngamia na mavazi; kisha akarejea na kufika kwa Akishi.