1 Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto;
2 nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wo wote, ila wakawachukua, wakaenda zao.
3 Basi Daudi na watu wake walipoufikilia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, waume kwa wake, wamechukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakainua sauti zao na kulia, hata walipokuwa hawana nguvu za kulia tena.
5 Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli.
6 Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana nafsi za hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika BWANA, Mungu wake.
7 Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko.