1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima wa Gilboa.
2 Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli.
3 Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde.
4 Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao; wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanichoma, na kunisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia.