1 Basi, hilo sanduku la BWANA lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba.
2 Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la BWANA? Tuonyesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake.
3 Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu.
4 Ndipo wakauliza, Na hayo matoleo ya kosa yatakuwa ya namna gani, hayo tutakayompelekea? Nao wakajibu, Na yawe majipu ya dhahabu matano, na panya wa dhahabu watano, sawasawa na idadi ya mashehe wa Wafilisti; kwa kuwa tauni moja ilikuwa juu yenu nyote, na juu ya mashehe wenu.
5 Kwa hiyo mtafanyiza sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu waiharibuo nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu.
6 Mbona, basi, mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya migumu mioyo yao? Hata na hao, hapo alipokwisha kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu, nao wakaenda zao?