1 Ikawa baada ya hayo, Daudi akauliza kwa BWANA, akasema, Je! Niupandie mji wo wote wa Yuda? BWANA akamwambia, Haya! Panda. Daudi akasema, Niupandie mji upi? Akasema, Hebroni.
2 Basi Daudi akapanda aende huko, pamoja na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mkewe Nabali, wa Karmeli.
3 Daudi naye akawapandisha watu wake waliokuwa pamoja naye, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; wakakaa katika miji ya Hebroni.
4 Basi watu wa Yuda wakaenda, wakamtia Daudi mafuta huko, awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda.Wakamwambia Daudi wakasema, Watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Sauli.
5 Basi Daudi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabesh-gileadi, na kuwaambia, Na mbarikiwe ninyi na BWANA, kwa kuwa mmemtendea bwana wenu fadhili hii, yaani Sauli, mkamzika.
6 BWANA naye sasa awatendee ninyi fadhili na kweli; mimi nami nitawalipeni fadhili hiyo, kwa sababu mmetenda jambo hilo.
7 Basi sasa, mikono yenu na itiwe nguvu, nanyi iweni mashujaa; maana Sauli, bwana wenu, amekufa, tena nyumba ya Yuda wamenitia mimi mafuta niwe mfalme juu yao.