1 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Moabu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu aliichoma moto mifupa ya mfalme wa Edomu hata ikawa chokaa; Sef 2:8-11; 2 Fal 3:27
2 lakini nitapeleka moto juu ya Moabu, nao utayateketeza majumba ya Keriothi; na Moabu atakufa pamoja na mshindo, na kelele, na sauti ya tarumbeta;
3 nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema BWANA.
4 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata;
5 lakini nitapeleka moto juu ya Yuda, nao utayateketeza majumba ya Yerusalemu.
6 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;