1 Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi.
2 Naye alisema,BWANA atanguruma toka Sayuni,Atatoa sauti yake toka Yerusalemu;Na malisho ya wachungaji yataomboleza,Na kilele cha Karmeli kitanyauka.
3 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma;
4 lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.
5 Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema BWANA.
6 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waliichukua katika hali ya kufungwa kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu;
7 lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake.
8 Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU.
9 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu;
10 lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake.
11 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararua-rarua daima, akaishika ghadhabu yake milele;
12 lakini nitapeleka moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra.
13 Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao;
14 lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela;
15 na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema BWANA.