1 Lisikieni neno hili alilolisema BWANA juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema,
2 Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote.
3 Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?
4 Je! Simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwana-simba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu?
5 Je! Ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu cho chote?
6 Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta BWANA?
7 Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.