13 Nao wakapita huko hata hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikilia nyumba ya huyo Mika.
14 Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakajibu, na kuwaambia ndugu zao Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya.
15 Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafikilia nyumba ya huyo hirimu, Mlawi, hata hiyo nyumba ya Mika, nao wakamwuliza habari za hali yake.
16 Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango.
17 Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita.
18 Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi?
19 Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli?