1 Ikawa katika siku hizo, hapo kulipokuwa hapana mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa hali ya ugeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda.
2 Kisha huyo suria yake akaandama ukahaba kinyume chake, kumwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa kuko muda wa miezi minne.
3 Kisha mumewe akainuka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda wawili; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye.
4 Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, akamzuia; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala kuko.
5 Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu.
6 Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi.
7 Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi-sihi, naye akalala kuko tena.
8 Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili.
9 Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu.
10 Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye.
11 Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tugeuke kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu.
12 Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea.
13 Kisha akamwambia mtumishi wake, Haya, tuifikilie miji hii mmojawapo nasi tutalala katika Gibea au katika Rama.
14 Basi wakashika njia kwenda zao mbele; jua likawachwea walipokuwa karibu na Gibea, ambao ni mji wa Benyamini.
15 Wakageuka huko, wapate kuingia na kulala katika Gibea; akaingia ndani, akaketi katika njia kuu ya mji; kwa kuwa hapakuwa na mtu awaye yote aliyewakaribisha nyumbani kwake kulala.
16 Kisha, tazama, akatokea mtu mume mzee, atoka kazini kwake shambani, wakati wa jioni; mtu huyo alikuwa ni wa ile nchi ya vilima vilima ya Efraimu, naye alikuwa anakaa katika Gibea hali ya ugeni lakini wenyeji wa mahali hapo walikuwa Wabenyamini.
17 Naye alipovua macho yake, akamwona huyo mtu msafiri katika njia kuu ya mji; huyo mzee akamwuliza, Waenda wapi wewe? Nawe watoka wapi?
18 Akamwambia, Sisi twapita hapa kutoka Bethlehemu-yuda, twaenda huko upande wa mbali wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu; ndiko nilikotoka nami nilikwenda Bethlehemu-yuda; nami sasa naiendea nyumba ya BWANA wala hapana mtu anikaribishaye nyumbani mwake.
19 Walakini nyasi tunazo, na chakula cha hawa punda zetu; mkate pia tunao na divai kwa mimi na huyu kijakazi wako, na kwa huyu kijana aliye pamoja nasi watumishi wako; hapana uhitaji wa kitu cho chote.
20 Kisha huyo mzee alisema, Na iwe amani kwako; lakini na haya yaliyokupungukia na yawe juu yangu mimi lakini usilale njiani.
21 Basi akamtia ndani ya nyumba yake, akawapa punda chakula; nao wakaosha miguu, wakala na kunywa.
22 Hapo walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, tazama, watu wa mji huo, watu mabaradhuli wakaizingira hiyo nyumba pande zote, wakagonga mlango; wakasema na huyo mwenye nyumba, huyo mzee, na kumwambia, Mlete nje mtu yule aliyefika nyumbani kwako, ili tupate kumjua.
23 Naye mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu.
24 Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii.
25 Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake.
26 Ndipo huyo mwanamke akaja alfajiri, akaanguka chini mlangoni pa nyumba ya mtu yule alimokuwamo bwana wake, hata kulipokucha.
27 Bwana wake akaondoka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aende zake, na tazama, huyo mwanamke suria yake alikuwa ameanguka pale mlangoni pa nyumba, na mikono yake ilikuwa i pale kizingitini.
28 Akamwambia, Haya ondoka, twende zetu; lakini hakuna aliyemjibu; ndipo akamwinua akamweka juu ya punda; mtu huyo akaondoka, akaenda mahali pake mwenyewe.
29 Naye alipokwisha kuingia nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika huyo suria yake, akampasua kiungo kwa kiungo, vipande kumi na viwili akampeleka katika mipaka yote ya Israeli.
30 Basi ikawa, wote walioliona jambo hilo wakasema, Jambo kama hili halijatendeka wala kuonekana tangu siku hiyo wana wa Israeli walipokwea kutoka katika nchi ya Misri hata leo; haya, lifikirini, fanyeni shauri, mkanene.