1 Kisha malaika wa BWANA alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi;
2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?
3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.
4 Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia.
5 Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia BWANA sadaka huko.
6 Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi.