12 Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika.
13 Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.
14 Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao.
15 Kila walikokwenda mkono wa BWANA ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama BWANA alivyosema, na kama BWANA alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.
16 Kisha BWANA akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara.
17 Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za BWANA bali wao hawakufanya hivyo.
18 Na wakati BWANA alipowainulia waamuzi, ndipo BWANA alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana BWANA alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.