1 Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya BWANA.
2 BWANA akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake.
3 Wana wa Israeli wakamlilia BWANA; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini.
4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule.
5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue.
6 Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! BWANA, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni?