31 Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako.
32 Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani;
33 kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi.
34 Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne.
35 Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia.
36 Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu.
37 Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu.