Dan. 5:15-21 SUV

15 Basi sasa, watu wenye hekima na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili.

16 Lakini nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme.

17 Ndipo Danieli akajibu, akasema mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.

18 Kwa habari zako, Ee mfalme, Mungu Aliye juu alimpa Nebukadreza, baba yako, ufalme, na ukuu, na fahari, na utukufu;

19 na kwa sababu ya ule ukuu aliompa, watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha, wakatetemeka na kuogopa mbele yake; aliyetaka kumwua alimwua; na aliyetaka kumwacha hai, alimwacha hai; aliyetaka kumtukuza, alimtukuza; na aliyetaka kumshusha, alimshusha.

20 Lakini moyo wake ulipoinuliwa, na roho yake ilipokuwa ngumu akatenda kwa kiburi, aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi, nao wakamwondolea utukufu wake.

21 Akafukuzwa mbali na wanadamu, moyo wake ukafanywa kuwa kama moyo wa mnyama, na makao yake yalikuwa pamoja na punda-mwitu; akalishwa majani kama ng’ombe, mwili wake ukalowa maji kwa umande wa mbinguni; hata alipojua ya kuwa Mungu Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu, na ya kuwa humweka juu yake yeye amtakaye, awaye yote.