1 Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.
2 Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa.
3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali.
4 Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.
5 Na tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.
6 Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.