45 Neno la BWANA likanijia, kusema,
46 Mwanadamu, uelekeze uso wako kusini, ukadondoze neno lako upande wa kusini, ukatabiri juu ya msitu wa uwanda wa Negebu,
47 ukauambie msitu wa Negebu, Lisikie neno la BWANA; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama nitawasha moto ndani yako, nao utakula kila mti mbichi ndani yako, na kila mti mkavu; miali ya moto ule haitazimika, na nyuso zote toka kusini hata kaskazini zitateketezwa kwa moto huo.
48 Na watu wote wenye mwili wataona ya kuwa mimi, BWANA, nimeuwasha; hautazimika.
49 Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, wao hunisema; Je! Mtu huyu si mtu mwenye kupiga mithali?