1 Neno la BWANA likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, kaza uso wako, umwelekee Gogu, wa nchi ya Magogu, mkuu wa Roshi, Mesheki, na Tubali, ukatabiri juu yake,
3 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Gogu, mkuu wa Roshi, na Mesheki, na Tubali;
4 nami nitakugeuza na kutia kulabu katika mataya yako, nami nitakutoa, pamoja na jeshi lako lote, farasi na hao wapandao farasi, wote wamevaa silaha za namna zote, jeshi kubwa sana, wenye ngao na kigao, wote wakishika upanga;
5 Uajemi, na Kushi, na Putu, pamoja nao; wote wana ngao na chapeo;
6 Gomeri, na vikosi vyake vyote; nyumba ya Togarma, pande za mwisho za kaskazini, na vikosi vyake vyote; naam, watu wengi pamoja nawe.
7 Ujiweke tayari, naam, jiweke tayari, wewe na majeshi yako yote waliokukusanyikia, nawe uwe jemadari wao.
8 Na baada ya siku nyingi utajiliwa; katika miaka ya mwisho, utaingia nchi iliyorudishiwa hali yake ya kwanza, baada ya kupigwa kwa upanga, iliyokusanywa toka kabila nyingi za watu, juu ya milima ya Israeli, iliyokuwa ukiwa wa daima; lakini imetolewa katika kabila za watu, nao watakaa salama salimini wote pia.
9 Nawe utapaa juu, utakuja kama tufani, utakuwa kama wingu kuifunika nchi, wewe, na vikosi vyako vyote, na kabila nyingi za watu pamoja nawe.
10 Bwana MUNGU asema hivi; Itakuwa katika siku hiyo, mawazo yataingia moyoni mwako, nawe utakusudia kusudi baya;
11 nawe utasema, Nitapanda juu niiendee nchi yenye vijiji visivyo na maboma; nitawaendea watu wanaostarehe, wanaokaa salama, wote wakikaa pasipo kuta, ambao hawana makomeo wala malango;
12 ili kuteka mateka, na kuwinda mawindo; uugeuze mkono wako juu ya mahali palipoharibika, ambapo sasa panakaliwa na watu, na juu ya watu waliokusanyika toka mataifa, waliopata ng’ombe na mali, wakaao katikati ya dunia.
13 Sheba, na Dedani, na wafanya biashara wa Tarshishi, pamoja na wana-simba wake wote, watakuambia, Je! Umekuja kuteka mateka? Umekusanya jeshi lako, ili kuwinda mawindo? Kuchukua fedha na dhahabu, kuchukua ng’ombe na mali, kuteka mateka mengi sana?
14 Basi, mwanadamu, tabiri, umwambie Gogu, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile watu wangu, Israeli, watakapokaa salama, hutapata habari?
15 Nawe utakuja kutoka mahali pako, kutoka pande za mwisho za kaskazini, wewe, na watu wa kabila nyingi pamoja nawe, wote wamepanda farasi, kusanyiko kubwa, na jeshi kuu;
16 nawe utapanda juu uwajilie watu wangu, Israeli, kama wingu kuifunika nchi; itakuwa katika siku za mwisho, nitakuleta upigane na nchi yangu, ili mataifa wanijue, nitakapotakaswa kwako, Ewe Gogu, mbele ya macho yao.
17 Bwana MUNGU asema hivi; Je! Wewe ndiwe niliyemnena zamani za kale, kwa vinywa vya watumishi wangu, manabii wa Israeli, waliotabiri siku zile kwa muda wa miaka mingi, ya kwamba nitakuleta upigane nao?
18 Itakuwa katika siku hiyo, Gogu atakapokuja kupigana na nchi ya Israeli, asema Bwana MUNGU, ghadhabu yangu itapanda katika mianzi ya pua yangu.
19 Kwa maana katika wivu wangu, na katika moto wa ghadhabu yangu, nimenena, Hakika katika siku ile kutakuwako tetemeko kubwa katika nchi ya Israeli;
20 hata samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama wa kondeni, na vitu vyote vitambaavyo juu ya nchi, na wanadamu wote walio juu ya uso wa nchi, watatetemeka mbele ya uso wangu; nayo milima itatupwa chini, na magenge yataanguka, na kila ukuta utaanguka chini.
21 Nami nitaita upanga, uje juu yake katika milima yangu yote, asema Bwana MUNGU; nao upanga wa kila mtu utakuwa juu ya ndugu yake.
22 Nami nitamhukumu kwa tauni, na kwa damu; nami nitanyesha mvua ifurikayo, na mvua ya mawe makubwa sana, na moto na kiberiti juu yake, na vikosi vyake, na watu wa kabila nyingi walio pamoja naye.
23 Nami nitajitukuza, na kujitakasa, na kujidhihirisha, mbele ya macho ya mataifa mengi; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.