20 Neno la BWANA likanijia, kusema,
21 Mwanadamu, uuelekezee Sidoni uso wako, ukatabiri juu yake,
22 useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Sidoni, nami natukuzwa kati yako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu ndani yake, na kutakasika ndani yake.
23 Maana nitampelekea tauni, na damu, katika njia kuu zake, na hao waliotiwa jeraha wataanguka kati yake, kwa upanga juu yake pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
24 Wala hautakuwapo mchongoma uchomao kwa nyumba ya Israeli; wala mwiba uumizao miongoni mwa wote wamzungukao, waliowatenda mambo ya jeuri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.
25 Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokuwa nimewakusanya nyumba ya Israeli, na kuwatoa katika watu ambao wametawanyika kati yao, na kutakasika kati yao machoni pa mataifa, ndipo watakapokaa katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu, Yakobo.
26 Nao watakaa humo salama; naam, watajenga nyumba, na kupanda mashamba ya mizabibu, na kukaa salama; nitakapokuwa nimetekeleza hukumu zangu juu ya watu wote, wanaowatenda mambo ya jeuri pande zote; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao.