11 Basi hii ndiyo nakala ya waraka, mfalme Artashasta aliyompa Ezra, kuhani, mwandishi, naam, mwandishi wa maneno ya amri za BWANA, na wa sheria zake alizowapa Israeli.
12 Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani, mwandishi wa torati ya Mungu wa mbinguni, salamu kamili; wakadhalika.
13 Natoa amri ya kwamba wote walio wa watu wa Israeli, na makuhani wao, na Walawi, katika ufalme wangu, wenye nia ya kwenda Yerusalemu kwa hiari yao wenyewe, waende pamoja nawe.
14 Kwa kuwa umetumwa na mfalme, na washauri wake saba, ili kuuliza habari za Yuda na Yerusalemu, kwa sheria ya Mungu wako iliyo mkononi mwako;
15 na kuichukua fedha na dhahabu, ambayo mfalme, na washauri wake, kwa hiari yao, wamemtolea Mungu wa Israeli, akaaye Yerusalemu;
16 na fedha yote na dhahabu utakayoona katika wilaya ya Babeli, pamoja na vitu watakavyotoa watu kwa hiari yao, na vitu vya makuhani walivyotoa kwa hiari yao, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.
17 Kwa sababu hiyo ujitahidi kununua kwa fedha hiyo mafahali, kondoo waume, wana-kondoo, pamoja na sadaka zao za unga, na sadaka zao za kinywaji; nawe utazitoa juu ya madhabahu ya nyumba ya Mungu wenu, iliyoko Yerusalemu.