1 Basi hawa ndio wakuu wa mbari za baba zao, na hii ndiyo nasaba ya wale waliokwea pamoja nami kutoka Babeli, wakati wa kutawala kwake mfalme Artashasta.
2 Wa wana wa Finehasi, Gershoni; wa wana wa Ithamari, Danieli; wa wana wa Daudi, Hatushi, mwana wa Shekania;
3 wa wana wa Paroshi, Zekaria; na pamoja naye wakahesabiwa kwa nasaba wanaume mia na hamsini.
4 Wa wana wa Pahath-Moabu, Eliehoenai, mwana wa Zerahia; na pamoja naye wanaume mia mbili;
5 Wa wana wa Zatu, Shekania, mwana wa Yahazieli; na pamoja naye wanaume mia tatu.
6 Na wa wana wa Adini, Ebedi, mwana wa Yonathani; na pamoja naye wanaume hamsini.
7 Na wa wana wa Elamu, Yeshaya, mwana wa Athalia; na pamoja naye wanaume sabini.
8 Na wa wana wa Shefatia, Zebadia, mwana wa Mikaeli; na pamoja naye wanaume themanini.
9 Wa wana wa Yoabu, Obadia, mwana wa Yehieli; na pamoja naye wanaume mia mbili na kumi na wanane.
10 Na wa wana wa Binui, Shelomithi, mwana wa Yosifia; na pamoja naye wanaume mia na sitini.
11 Na wa wana wa Bebai, Zekaria, mwana wa Bebai; na pamoja naye wanaume ishirini na wanane.
12 Na wa wana wa Azgadi, Yohana, mwana wa Hakatani; na pamoja naye wanaume mia na kumi.
13 Na wa wana wa Adonikamu, hawa waliokuwa wa mwisho, na hayo ndiyo majina yao, Elifeleti, na Yeueli, na Shemaya; na pamoja nao wanaume sitini.
14 Na wa wana wa Bigwai, Uthai, mwana wa Zabudi; na pamoja naye wanaume sabini.
15 Nikawakusanya penye mto ushukao kwenda Ahava; na huko tukapiga kambi yetu muda wa siku tatu; nikawakagua watu, na makuhani, wala sikuona hapo wana wa Lawi hata mmoja.
16 Ndipo nikatuma watu kwenda kumwita Eliezeri, na Arieli, na Shemaya, na Elnathani, na Yaribu, na Elnathani, na Nathani, na Zekaria, na Meshulamu, waliokuwa wakuu; na Yoyaribu, na Elnathani pia, waliokuwa waalimu.
17 Nikawapeleka kwa Ido, mkuu, huko Kasifia; nikawaambia watakayomwambia Ido, na ndugu zake hao Wanethini, huko Kasifia, kwamba watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu wetu.
18 Na kama mkono mwema wa Mungu wetu ulivyokuwa pamoja nasi, wakamletea Ishekeli, mmoja wa wana wa Mali, mwana wa Lawi, mwana wa Israeli; na Sherebia, pamoja na wanawe na ndugu zake, watu kumi na wanane;
19 na Hashabia, na pamoja naye Yeshaya, wa wana wa Merari, na ndugu zake na wana wao, watu ishirini;
20 na katika Wanethini, ambao Daudi, na wakuu, walikuwa wamewaweka kwa ajili ya utumishi wa Walawi, Wanethini mia mbili na ishirini; wote wametajwa kwa majina yao.
21 Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote.
22 Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao.
23 Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.
24 Ndipo nikawatenga watu kumi na wawili wa wakuu wa makuhani, nao ni Sherebia, na Hashabia, na watu kumi wa ndugu zao pamoja nao,
25 nami nikawapimia kwa mizani zile fedha, na dhahabu, na vile vyombo, matoleo kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu, ambayo mfalme, na washauri wake, na wakuu wake, na Israeli wote waliokuwapo, walikuwa wameyatoa;
26 nami nikawapimia mikononi mwao talanta za fedha mia sita na hamsini na vyombo vya fedha talanta mia; na talanta mia za dhahabu;
27 na mabakuli ishirini ya dhahabu, thamani yake darkoni elfu; na vyombo viwili vya shaba nzuri iliyong’aa, thamani yake sawa na dhahabu.
28 Kisha nikawaambia, Ninyi mmekuwa watakatifu kwa BWANA, na hivyo vyombo ni vitakatifu; na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa BWANA, Mungu wa baba zenu.
29 Basi, angalieni, na kuvitunza vitu hivi, hata mtakapovipima mbele ya wakuu wa makuhani, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli, huko Yerusalemu, katika vyumba vya nyumba ya BWANA.
30 Hivyo makuhani na Walawi wakaupokea uzani wa fedha, na dhahabu, na vyombo, ili kuvileta Yerusalemu nyumbani kwa Mungu wetu.
31 Ndipo tukasafiri toka mtoni Ahava siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, ili kwenda Yerusalemu; na mkono wa Mungu ulikuwa pamoja nasi, akatuokoa na mkono wa adui, na mtu mwenye kutuvizia njiani.
32 Tukafika Yerusalemu, tukakaa huko muda wa siku tatu.
33 Hata siku ya nne, hizo fedha na dhahabu na vile vyombo vilipimwa ndani ya nyumba ya Mungu, vikatiwa mikononi mwa Meremothi, mwana wa Uria, kuhani; na pamoja naye alikuwapo Eleazari, mwana wa Finehasi; na pamoja nao Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui, Walawi;
34 vile vyombo vyote kwa hesabu na kwa uzani; tena uzani wake wote uliandikwa wakati ule.
35 Na wana wa uhamisho, waliokuwa wametoka katika uhamisho wakamtolea Mungu wa Israeli sadaka za kuteketezwa, ng’ombe kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, na kondoo waume tisini na sita, na wana-kondoo sabini na saba, na mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi, hao wote pia walikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.
36 Wakawapa manaibu wa mfalme, na maliwali wa ng’ambo ya Mto, maagizo ya mfalme; nao wakawapa watu, na nyumba ya Mungu, msaada.