5 Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu.
6 Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake.
7 Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa.
8 Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye aliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali.
9 Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake.
10 Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu.
11 Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa.