1 Usifurahi, Israeli, kwa sababu ya furaha, kama hao mataifa; kwa kuwa umezini juu ya Mungu wako, umependa ujira katika kila sakafu ya nafaka.
2 Sakafu na shinikizo hazitawalisha, na divai mpya itampungukia.
3 Hawatakaa katika nchi ya BWANA; lakini Efraimu atarudi Misri, nao watakula chakula kinajisi katika Ashuru.
4 Hawatammiminia BWANA divai, wala hazitampendeza sadaka zao; mkate wao utakuwa kama chakula cha matanga kwao; wote watakaokila watatiwa unajisi; kwa maana mkate wao utakuwa kwa shauku zao; hautaingia katika nyumba ya BWANA.
5 Mtafanya nini katika siku ya mkutano wa idi, na katika siku ya karamu ya BWANA?
6 Kwa maana, tazama, wamekwenda zao ili kukimbia uharibifu, lakini Misri itawakusanya, Nofu itawazika; vitu vyao vya fedha viwapendezavyo, magugu yatavimiliki; miiba itakuwa katika hema zao.
7 Siku za kupatilizwa zimekuja, siku za kulipa zimefika; Israeli atayajua hayo; huyo nabii ni mpumbavu, huyo mtu mwenye roho ana wazimu; kwa sababu ya wingi wa uovu wako, na kwa sababu uadui umekuwa mkubwa.