16 Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, BWANA, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri;
17 Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.
18 Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, BWANA Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu BWANA Mungu wetu.
19 Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu.
20 Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.
21 Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu;
22 Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.