1 BWANA akasema na Musa, akamwambia,
2 Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo.
3 Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa BWANA aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa.
4 Ninyi mwatoka leo katika mwezi wa Abibu.
5 Itakuwa hapo BWANA atakapowaleta mpaka nchi ya Wakanaani, na Wahiti, na Waamori, na Wahivi, na Wayebusi, nchi hiyo aliyowaapia baba zako kwamba atakupa wewe, ni nchi imiminikayo maziwa na asali, ndipo mtakapoushika utumishi huu katika mwezi huu.
6 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba, nayo siku ya saba itakuwa ni sikukuu ya BWANA.
7 Mikate isiyochachwa italiwa katika hizo siku saba; mkate uliotiwa chachu usionekane kwako, wala chachu isionekane kwako, ndani ya mipaka yako yote.
8 Nawe utamwambia mwanao siku hiyo, ukisema, Ni kwa sababu ya hayo BWANA aliyonifanyia hapo nilipotoka Misri.
9 Nayo itakuwa ishara kwako katika mkono wako, na kwa ukumbusho kati ya macho yako, ili kwamba sheria ya BWANA ipate kuwa kinywani mwako; kwani BWANA alikutoa utoke Misri kwa mkono wenye uwezo.
10 Kwa hiyo utaitunza amri hii kwa wakati wake mwaka baada ya mwaka.
11 Itakuwa hapo BWANA atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, kama alivyokuapia wewe na baba zako, na kukupa,
12 ndipo utamwekea BWANA kila afunguaye tumbo, na kila mzaliwa wa kwanza uliye naye, azaliwaye na mnyama; hao waume watakuwa ni wa BWANA.
13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; na kwamba hutaki kumkomboa, utamvunja shingo; na kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu katika wanao utamkomboa.
14 Kisha itakuwa hapo mwanao atakapokuuliza keshoni, akisema, Ni nini hivi? Utamwambia, BWANA alimtoa Misri, kutoka ile nyumba ya utumwa, kwa uwezo wa mkono wake;
15 basi ilikuwa hapo Farao alipojifanya kuwa mgumu ili asitupe ruhusa kuondoka, BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote waliokuwa katika nchi ya Misri, wa binadamu na wa mnyama; kwa ajili ya hayo namtolea BWANA wote wafunguao tumbo, wakiwa waume; lakini wazaliwa wa kwanza wote wa wana wangu nawakomboa.
16 Jambo hilo litakuwa ni ishara mkononi mwako, na utepe katikati ya macho yako; kwa kuwa BWANA alitutoa Misri kwa uwezo wa mkono wake.
17 Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri;
18 lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.
19 Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.
20 Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa.
21 BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;
22 ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.