1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,Kabla hazijaja siku zilizo mbaya,Wala haijakaribia miaka utakaposema,Mimi sina furaha katika hiyo.
2 Kabla jua, na nuru, na mwezi,Na nyota, havijatiwa giza;Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
3 Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema;Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha;Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba;Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza;
4 Na milango kufungwa katika njia kuu;Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo;Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege;Nao binti za kuimba watapunguzwa;
5 Naam, wataogopa kilichoinukaNa vitisho vitakuwapo njiani;Na mlozi utachanua maua;Na panzi atakuwa ni mzigo mzito;Na pilipili hoho itapasuka;Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele,Nao waombolezao wazunguka njiani.
6 Kabla haijakatika kamba ya fedha;Au kuvunjwa bakuli la dhahabu;Au mtungi kuvunjika kisimani;Au gurudumu kuvunjika birikani;
7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa,Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.