13 Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao.
14 Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake.
15 Siku hizo naliona katika Yuda watu wengine waliokanyaga mashinikizo ya mvinyo siku ya sabato, na wengine waliochukua miganda, na kuwapakia punda zao; tena na mvinyo, na zabibu, na tini, na namna zote za mizigo, waliyoileta Yerusalemu, siku ya sabato; nami nikashuhudia juu yao siku ile waliyouza vyakula.
16 Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki, na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo Yerusalemu.
17 Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato?
18 Je! Sivyo hivyo walivyofanya baba zenu; na Mungu wetu, je! Hakuyaleta mabaya haya yote juu yetu, na juu ya mji huu? Nanyi hata hivyo mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato!
19 Ikawa malango ya Yerusalemu yalipoanza kuwa na giza kabla ya sabato, naliamuru milango ifungwe, nikaamuru isifunguliwe hata sabato iishe; na baadhi ya watumishi wangu nikawaweka juu ya malango, ili usiingizwe mzigo wo wote siku ya sabato.