11 Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.
12 Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.
13 Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.
14 Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati sawasawa na hayo matendo yao, na yule nabii mke Noadia, na hao manabii waliosalia, waliotaka kuniogofya.
15 Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.
16 Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo makafiri wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.
17 Tena siku zile wakuu wa Yuda walimletea Tobia nyaraka nyingi, nazo nyaraka za Tobia zikawafikilia.