29 ukawashuhudia ili uwarudishe tena katika sheria yako; lakini walitakabari, wasizisikilize amri zako, bali wakazihalifu hukumu zako, (ambazo mtu akizitenda ataishi katika hizo), nao wakayaondoa mabega yao, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wasitake kusikiliza.
30 Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.
31 Ila kwa rehema zako nyingi hukuwakomesha kabisa, wala kuwaacha; kwa maana wewe u Mungu mwenye neema, mwenye rehema.
32 Basi sasa, Ee Mungu, mkuu, mwenye uweza, Mungu wa kuogofya, mwenye kushika maagano na rehema, mashaka yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na manabii wetu, na baba zetu, na watu wako wote, tangu zamani za wafalme wa Ashuru hata leo, na yasihesabiwe kuwa ni madogo.
33 Lakini wewe u mwenye haki, katika hayo yote yaliyotupata; maana wewe umetenda yaliyo kweli, lakini sisi tumetenda yaliyo mabaya;
34 na wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na baba zetu, hawakuishika sheria yako, wala hawakuzisikiliza amri zako na shuhuda zako, ulizowashuhudia.
35 Kwa kuwa hawakukutumikia wewe katika ufalme wao, na katika wema wako mkuu uliowapa, na katika nchi ile kubwa yenye neema uliyowapa mbele yao, wala hawakughairi na kuyaacha mabaya yao.