8 Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake.
9 Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi.
10 Tena, huyu Ruthu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi.
11 Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. BWANA na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu.
12 Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa BWANA katika mwanamke huyu.
13 Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na BWANA akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume.
14 Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe BWANA, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli.