2 siku ya giza na weusi, siku ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi.
3 Moto unakula mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Adeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao.
4 Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio.
5 Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto ilapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita.
6 Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu.
7 Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao.
8 Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyizia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao.