3 Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA.
4 Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.
5 Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.
6 Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.
7 Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.
8 Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?
9 Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.