1 Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika.
2 Akamwomba BWANA, akasema, Nakuomba, Ee BWANA; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya.
3 Basi, sasa, Ee BWANA, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
4 Naye BWANA akasema, Je! Unatenda vema kukasirika?
5 Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje.
6 Na BWANA Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango.