3 Kwangu mimi si kitu nikihukumiwa na nyinyi, au na mahakama ya kibinadamu; wala sijihukumu mimi mwenyewe.
4 Dhamiri yangu hainishtaki kwa jambo lolote, lakini hiyo haionyeshi kwamba sina lawama. Bwana ndiye anayenihukumu.
5 Basi, msihukumu kabla ya wakati wake; acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yaliyofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu. Ndipo kila mmoja atapata sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.
6 Ndugu, hayo yote niliyosema juu ya Apolo na juu yangu, ni kielelezo kwenu: Kutokana na mfano wangu mimi na Apolo nataka mwelewe maana ya msemo huu: “Zingatieni yaliyoandikwa.” Kati yenu pasiwe na mtu yeyote anayejivunia mtu mmoja na kumdharau mwingine.
7 Nani amekupendelea wewe? Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukukipewa?
8 Haya! Mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tutawale pamoja nanyi.
9 Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu.