25 Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa.
26 Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo.
27 Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa.
28 Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate nyinyi.
29 Ndugu, nataka kusema hivi: Muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa;
30 wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu;
31 nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita.