3 Watu watakapokuwa wanasema: “Kila kitu ni shwari na salama”, ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.
4 Lakini nyinyi, ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.
5 Nyinyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.
6 Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.
7 Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.
8 Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.
9 Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo