3 Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua.
4 Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake.
5 Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye:
6 Mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.
7 Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia.
8 Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa kweli umekwisha anza kuangaza.
9 Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani.