10 Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena,
11 nyinyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.
12 Sisi tunajivunia kitu kimoja: Dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali na neema ya Mungu.
13 Tunawaandikia nyinyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa,
14 maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea nyinyi fahari.
15 Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.
16 Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.