27 Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.
28 Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!
29 “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa.
30 Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo.
31 Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada.
32 “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme.
33 Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.