8 “Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate.
9 Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’
10 Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.”
11 Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume.
12 Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake.
13 Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo.
14 Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika.