24 Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.
25 “Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.
26 Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.
27 Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.
28 Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.”
29 Kisha akawaambia mfano: “Angalieni mtini na miti mingine yote.
30 Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba majira ya mavuno yamekaribia.