1 Yesu akaendelea kuwaambia, “Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa enzi.”
2 Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao,
3 mavazi yake yakangaa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe.
4 Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu.
5 Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.”
6 Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema.
7 Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.”