5 Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu.”
6 Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani.
7 Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha.
8 Kwa kujitetea, Paulo alisema, “Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu sheria ya Wayahudi, wala kuhusu hekalu, wala kumhusu Kaisari.”
9 Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?”
10 Paulo akajibu, “Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari, na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote.
11 Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!”