10 Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyemwongoza wakati aliposema.
11 Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu.”
12 Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na waalimu wa sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza Kuu.
13 Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, “Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na sheria ya Mose.
14 Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose.”
15 Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.