29 “Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyanganya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyanganya mali yake.
30 “Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
31 Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu.
32 Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao.
33 “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mazuri; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake.
34 Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali nyinyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni.
35 Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya.