1 Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Ni nani aliye mkubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni?”
2 Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao,
3 kisha akasema, “Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
4 Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
5 Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi.
6 “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari.
7 Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.