33 Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda hadi nchi ya mbali.
34 Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake.
35 Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamuua na mwingine wakampiga mawe.
36 Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile.
37 Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: ‘Watamjali mwanangu.’
38 Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: ‘Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!’
39 Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.